Monday, 30 September 2013

Sheikh Azzan: “Viongozi wawe waadilifu”

                                                                  Picha hii ya mwezi Juni 2012 inawaonesha viongozi wa Jumuiya ya Uamsho ambao hivi sasa wako ndani . Kutoka kulia ni Sheikh Azzan Hamdan (kulia, ametolewa kwa dhamana ya matibabu), Sheikh Farid Hadi na Maalim Mussa Juma (bado wako ndani).                                                                                                                           MAPEMA Jumamosi asubuhi Sheikh Azzan Khalid Hamdan, kiongozi mwandamizi wa Jumuiya ya 
Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, alizungumza na Zanzibar Daima Online nyumbani kwake Mfenesini, Unguja.
Na Ahmed Rajab
ALIITIKIA simu yangu kwa upole na unyenyekevu bila ya kukasirika kwamba nilimsumbua kwa simu mara tu baada ya swala ya alfajiri.  Nilimwambia niko tayari kwenda aliko ili tuzungumze. Hakunikatalia.
Alinielekeza kwamba tukishafika kwenye Mahakama ya Mfenesini tutazikuta nyumba zake nyuma ya maduka.  Kulikuwa kumekwishapambazuka nilipowasili na mwenzangu na majirani zake Sheikh Azzan waliojaa bashasha walitusalimia vizuri na kutuonyesha nyumba zake mbili.
Tuliposogea karibu watu wake wa nyumbani walituambia ni ipi kati ya hizo mbili alimokuwamo Sheikh Azzan.  Tulimkuta amekaa chini na hakuweza kusimama kutusalimia kwa maumivu yanayosababishwa na mawe kwenye mafigo yake.
Alitutaka radhi mara mbilimbili kwani alihisi alifanya utomvu wa adabu kutusalimia bila ya kusimama.
Alizidi kunitaka radhi kwani tulikuwa tumepanga tukutane jana Magharibi nikafika tulikoagana lakini sikumkuta.
azzan1
Sheikh Azzan Khalid Hamdan ambaye kwa sasa yuko nje kwa dhamana ya matibabu.
“Watu wengi sana walikuwa wakija kiasi cha kunifanya nichanganyikiwe na nikasahau kama tuliagana,” Sheikh Azzan alinambia.
Hao watu wengi walikuwa wakienda kumpa ‘stahil salama’ kwani saa chache tu kabla hapo jana (Ijumaa) Jaji Mkuu Omar Othman Makungu akiwa katika Mahakama ya Vuga aliamua kuwa Sheikh Azzan aachiwe kwa dhamana ili aweze kwenda ng’ambo kwa matibabu.
Sheikh Azzan mwenyewe hakuwako Mahakamani wala hakuwepo gerezani alikokuwa ameshikwa pamoja na viongozi wengine wa Uamsho. Alikuwa bado amelazwa kwenye Spitali ya Mnazi Mmoja.
Tukiyaacha mawe katika figo zake, Sheikh Azzan anatatizwa pia na ukosefu wa usingizi.
“Sipati usingizi usiku wala mchana.  Pia nina ulcer na mara nyingi hukimbilia spitali.  Nimepoteza fahamu mara tano — mara mbili gerezani na mara tatu spitali,” alisema Sheikh Azzan.
Nilimuuliza kuhusu hali za wenzake waliobaki gerezani.
“Wazima isipokuwa wana matatizo madogo madogo ya kiafya,” alisema Sheikh Azzan anayetarajia kwenda India kwa matibabu Jumanne ijayo.
Akieleza hali za gerezani za wafungwa wenzake, Sheikh Azzan alisema kwamba wanaachiwa kuwa pamoja.  Watu kumi wanaswali pamoja swala za adhuhuri na alasiri.
“Swala za isha, maghribi na alfajiri huswaliwa na watu watatu watatu,” alisema Sheikh Azzan na akaongeza kuwa kuna mtu mmoja, Mzee Suleiman Juma.
Je, alipata fununu yoyote kwamba ataachiwa jana?
“Nilikuwa na tamaa lakini nilishangaa nilipoona kwamba masharti si magumu ni ya kawaida”, alieleza Sheikh Azzan.
Hata hivyo, siku hizi kwa mujibu wa Sheikh Azzan hali ya mambo gerezani imebadilika kidogo.  Yeye na wenzake wamekuwa wakiruhusiwa kupata chakula kutoka makwao pamoja na magazeti.
“Tuna nafuu kubwa sio kama mwanzo.  Zamani tukiwekwa katika mazingira ya kila mtu abakie chumbani mwake kwa muda wa siku 42,” alisema Sheikh Azzan.
Aliongeza kusema siku hizi wao wafungwa wana maelewano mazuri na watu wa magereza na kwamba hao watu wa magereza, kwa hakika, wanasaidia sana.
Sheikh Azzan aliyakhitimisha mazungumzo yetu kwa kuwashukuru Wazanzibari na Waislamu wote, kwa jumla, kwa kuwa pamoja nao viongozi wa Uamsho walio korokoroni.  Aliwasihi waendelee kumuombea dua.
Watu wengi, alisema, wamejitolea kumsaidia kugharimia matibabu yake huko India.  Inavyosemekana ni kwamba zinahitajiwa shilingi milioni 16 kwa matibabu hayo.
Sheikh Azzan alikuwa na ujumbe maalum kwa viongozi wa Serikali.  Alisema viongozi hao wanapaswa wawe waadilifu.
“Sisi raia wa kawaida na wa halali.  Hatukatai kushtakiwa lakini watufanyie uadilifu.  Tunaiomba Serikali iharakishe hii kesi.  Muda umekwishakuiwa mkubwa.  Mheshimiwa Rais [Ali Mohamed Shein] alikula kiapo kuwa atakuwa mwadilifu basi awe mwadilifu,” alisihi Sheikh Azzan.
“Kwa upande mwingine naishukuru Serikali kwa kulifikiria ombi langu na Mahakama kwa kutenda uadilifu kwa kutoniwekea pingamizi,” alimaliza Sheikh Azzan.
Kesi ya washtakiwa wa Uamsho inatarajiwa kusikilizwa tena Oktoba 7.

0 comments:

Post a Comment